September 25, 2010

Waziri Sonyo Afungwa

Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Tanga, jana ilimtia hatiani mwanamuziki wa zamani wa bendi za TOT Plus ‘Achimenengule’, Chuchu Sound na African Revolution, Waziri Sonyo (35) na kumpa adhabu ya kifungo cha nje cha miaka miwili kwa kupatikana na hatia ya kukutwa na pikipiki ya wizi.

Akisoma hukumu hiyo jana, hakimu wa mahakama hiyo, Liberatus Mbuya, alisema kuwa, katika kipindi hicho cha kutumikia adhabu, Sonyo hatakiwi kutenda kosa lolote.

Awali, katika kesi hiyo ya Septemba 2009, Sonyo na washitakiwa wengine wawili ambao ni Ally Saidi (27) na Mohamed Mabranto, walishitakiwa kwa tuhuma za kula njama na kuiba pikipiki aina ya Yamaha CC200, yenye namba za usajili DFP 5974, tukio lililohusisha matumizi ya silaha.

Ilidaiwa kuwa Sonyo na wenzake walitenda kosa hilo kati ya Septemba 3 hadi 5 mwaka jana, na kwamba pikipiki hiyo ilikuwa na thamani ya Sh. 6,500,000, katika eneo la Chumbageni jijini Tanga.

Hata hivyo, mahakama hiyo ilimwachia huru mtuhumiwa wa pili katika kesi hiyo, Mohamed Mabranto, kwa madai kuwa mahakama hiyo haikupata ushahidi wa kutosha wa kumtia hatiani, huku mshitakiwa wa tatu, Waziri Sonyo, akitiwa hatiani kwa kosa la kukutwa na mali hiyo ya wizi.

Wanasheria wa Serikali, Jenifer Kaaya na Hilda Kato walieleza kuwa, mtuhumiwa wa kwanza Ally Saidi (27) mkazi wa barabara ya saba jijini hapa, alitorokea kusikojulikana.

Awali, wakisomewa mashitaka yao Septemba mwaka jana, ilidaiwa kuwa, Mwanamuziki huyo ambaye ni mkazi wa Majani Mapana katika jiji la Tanga, akiwa na wenzake, waliwatishia walinzi wa eneo hilo, Mwajabu Ernest na Jacob Manase kwa silaha za panga na nondo walizokuwa wamebeba na hatimaye wakafanya uhalifu huo.

CHANZO: NIPASHE

No comments:

Post a Comment