September 04, 2010

Mkoloni Anusurika Kumuona Pilato

MwanaHip Hop mwenye damu ya harakati za kutetea haki, Fred Maliki ‘Mkoloni’ amenusurika kifo baada ya kulishwa chakula chenye sumu.Habari zisizo na shaka zinasema kuwa Mkoloni alikula mtori unaoaminika uliwekewa sumu, Jumatano iliyopita kwenye baa moja maarufu iliyopo Sinza, Dar es Salaam.


Kwa mujibu wa rafiki wa Mkoloni, Gerald Mwanjoka ‘G Solo’ aliyeshuhudia ‘ishu’ nzima, mwanamuziki huyo baada ya kula mtori huo, alipelekwa Hospitali ya Palestina, Sinza na iliposhindikana alihamishiwa Hospitali ya Mkoa wa Kinondoni, Mwananyamala.

Alisema, alipigiwa simu asubuhi ili wakutane na kupanga mikakati ya kuendelea kufanya kampeni za kumuwezesha rafiki yao, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ ashinde ubunge Jimbo la Mbeya Mjini.

“Tulikutana barabarani jirani na baa hiyo. Tukaona tuingie ndani ili kuzungumza vizuri,” alisema G Solo na kuongeza:
“Sisi wote tulikuwa hatujala tangu asubuhi, Mkoloni akamwita mhudumu akaniambie niagize, mimi nikaagiza supu. Yule mhudumu aliporudi alikuja na mtori.

“Mkoloni akamwambia yule mhudumu ni kwanini ameleta mtori wakati nilimuagiza supu, yule mhudumu akasema supu imeisha. Mimi nikaona siyo kitu. Nikachukua huo mtori na kuanza kuushughulikia.

“Hapo hapo Mkoloni akaagiza na yeye mtori, alipoletewa na kuanza kula baada ya muda alianza kulalamika kichwa kinamuuma, akasema macho hayaoni akaanza na kutapika. Nikamuuliza kulikoni akasema hali ni mbaya nimpeleke kwa mchungaji amuombee.

“Nilimpakia kwenye gari hadi kwa mchungaji ambaye alimuombea lakini akawa anaendelea kukosa nguvu. Tukampa maziwa akayatapika, akaendelea kuwa na hali mbaya mpaka akapoteza fahamu.”

G Solo alisema kuwa baada ya Mkoloni kupoteza fahamu, alimpeleka Hospitali ya Palestina ambako aliwekewa ‘dripu’ kwa dakika kadhaa kabla ya kuhamishiwa Mwananyamala.

“Kule Palestina hawakusema kitu ila Mwananyamala daktari alisema kama siyo sumu basi aliwekewa dawa za kulevya kali, kwahiyo zilikuwa zinakwisha nguvu kadiri anavyowekewa dripu.

“Tulikwenda polisi lakini wakasema tulitakiwa kumpeleka pale pale alipopata matatizo ili mtori upimwe au matapishi yake yapimwe. Kwahiyo upande wa polisi tumeishia hapo,” alisema G Solo.

Gazeti hili lilitembelea Mkoloni Hospitali ya Mwananyalamala, Dar Jumatano iliyopita ambapo mpaka usiku, alikuwa bado hajapata fahamu za kutosha.

Alhamisi asubuhi, gazeti hili lilirudi tena hospitalini hapo na kumuona katika maendeleo mazuri, ingawa hakuwa na nguvu za kutosha.

Alipoulizwa hali yake, Mkoloni alisema: “Naendelea vizuri lakini nasuasua.”
Mkoloni aliyenza kuwika kwenye Bongo Flava akiwa na Kundi la Wagosi wa Kaya, hivi karibuni alizua mzozo baada ya kurekodi nyimbo za kuwashambulia watu wanaodai wanaua muziki wa kizazi kipya katika mradi ambao waliupa jina la Anti Virus.

Alipopata matataizo hayo, ilikuwa ni siku tatu tangu aliposoma risala inayoelezea jinsi wanamuziki wanavyonyonywa na kundi fulani katika uzinduzi wa kampeni za Urais, Ubunge na Udiwani za CHADEMA kwenye Uwanja wa Jangwani, Dar Jumamosi iliyopita.

No comments:

Post a Comment