November 27, 2011

SUGU Na VINEGA Waitetemesha Dar


Mamia ya mashabiki wa muziki wa kizazi kipya wakiongozwa na Mbunge wa Hai, Freeman Mbowe, Mbunge wa Ilemela Hynes Kiwia na Mbunge wa Jimbo la Ubungo John Mnyika (CHADEMA) juzi walifurika katika viwanja vya Ustawi wa jamii
na kushuhudia uzinduzi wa albamu ya pili ya Anti Virus.

Shangwe zilianza tangu mwanzo wa shoo hiyo wakati msanii wa muziki huo, Sista P alipopanda stejini na kuimba wimbo wake wa "Anakuja" ambao uliwafanya mashabiki hao kulipuka kwa mayowe huku wengine wakipuliza vuvuzela walizokuwa nazo.

Daz Mwalimu aliwakilisha kundi la Daz Nundaz kabla ya kundi la Mabaga Fresh, Mapacha, Nandul Mobb, Hard Mad, Danny Msimamo Rama D, Nuru Elly na Zay B kupanda ambao nao pia walishangiliwa ipasavyo na kuonyesha kuwa pamoja kuwa walikuwa mafichoni kwa muda mrefu bila kutoa nyimbo mpya bado wanapendwa.

Mashabiki walizidi kupagawa pale alipopanda mmoja wa viongozi wa kundi la Vinega, Adili Mkwela ambaye aliingia na kuimba wimbo wake wa siku nyingi wa 'Peke Yangu' ambao ulizidi kuamsha shangwe kutoka kwa mashabiki ambao walimtaka aurudie wimbo huo kwa madai kuwa ulikuwa ni maalumu kwa wale waliowasaliti wasanii hao.

Soggy Dogg Hunter alionyesha kuwa 'Kibanda cha Simu' na 'Nilikaona Mwaka Jana' bado ni nyimbo bora nchini wakati aliposhusha shoo ya nguvu iliyowafanya mashabiki wake kuzidi kupagawishwa na msanii huyo ambaye pia ni mtangazaji wa redio jijini Dar es Salaam.

Funga kazi ilikuwa pale ilipotangazwa kuwa mkongwe wa muziki huo, mwanaharakati na Mbunge wa Jimbo la Mbeya Mjini, Joseph Mbilinyi ‘Sugu’ kuwa anaingia stejini. Ilikuwa ni raha ambayo iliwafanya baadhi ya mashabiki waliokuwepo kumwagika machozi ya furaha kutokana na hamu ya kumuona waliyokuwanayo.

Sugu baada ya kuingia stejini majira ya saa 6:25 alianza kuwapagawisha wapenzi wake kwa wimbo wa 'Sugu Moto Chini', 'Chini ya Miaka 18', 'Wanataka Upate Tabu' na kumalizia na 'Mambo ya Fedha' ambao ulizidi kuwachanganya mashabiki hao ambao muda wote walionekana wakipunga mikono hewani huku wengine wakionyesha hewani kitabu alichotunga Sugu na wengine wakionyesha mabango yao hewani likiwemo lililosomeka: "Sugu Mwanahakati Anayesalitiwa na Anaowatetea".

Baada ya kumaliza nyimbo hizo, Sugu, ambaye alionekana kuwa na pumzi licha ya kuanza kuzoea vikao vya Bunge, aliamua kusimama kwa muda ili kuwatambulisha wananchi hao uwepo wa wabunge Mnyika na mwenzake Kiwia ambapo walipata nafasi ya kuzungumza kwa sekunde chache kwa kuwasalimia mamia ya mashabiki waliokuwemo na kisha kuondoka na kuwa watazamaji na kumpisha Sugu akiendelea kupagawisha.

Baada ya wabunge hao kushuka, Sugu aliendelea kufanya vitu vyake kwa kuimba wimbo wake wa mapenzi uliobeba jina la 'Yale Hayakuwa Mapenzi' ambao ulionyesha kuvuta hisia za mashabiki wengi waliokuwemo humo kwani walikaa kimya wakisikiliza mashairi kabla ya kuwaleta "Wananiita Sugu".

Wimbo huo ulimfanya mbunge huyo kuimba hatua kwa hatua na mashabiki wake hadi mwisho na alipomaliza walianza kupiga kelele wakitaka arudie tena wimbo huo, lakini aliwakatiza kwa kuwaambia: "ngojeni kwanza mashabiki wangu nataka niwatambulishe msanii nitakayemshirikisha kwenye albamu yangu ijayo, naomba taa zizimwe."

Taa zilipowashwa dakika chache baadaye ikiwa ni muda wa saa 7:15, shangwe zililipuka baada ya kuonekana stejini mkuu wa kambi ya upinzani bungeni, Freeman Mbowe ambaye aliwasalimia wapenzi hao akisema: "Asante kwa kuja hapa kumuunga mkono Sugu, naomba muendelee kumuunga mkono, najua muda umeenda sana lakini naomba wana usalama mliokuwepo hapa mumuache Sugu aendelee kwa dakika 10 na baada ya hapo naowamba muondoke kwa amani," alisisitiza Mbowe.

Mara baada ya kushuka EXTRA FLAVA ilizungumza na Mbowe kuhusu tamasha hilo ambapo alisema kuwa muziki unasaidia kuunganisha watu na kuwasaidia watu kuondoa matatizo mbalimbali waliyokuwa nayo.

"Hii sio siasa ni burudani kama burudani nyingine, inakusanya watu wa rika lote na watu kama akina Sugu wanahitajika sana kwani kwa kufanya hivi wanadhihirishia umma wa Watanzania kuwa muziki sio uhuni, sio umalaya bali ni kazi kama ilivyo kazi nyingine, na ndio maana Sugu ameonyesha kwa vitendo," alisema Mbowe

No comments:

Post a Comment