November 27, 2011

CHADEMA Wakutana Na Rais Ikulu!!


Rais Jakaya Kikwete, jana alikutana na viongozi waandamizi wa Chama Cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) na kufanya nao mazungumzo ikiwa ni kutekeleza ahadi yake ya kukutana nao baada ya chama hicho kuomba kuonana naye..



Rais Kikwete alikutana na viongozi wa Chadema Ikulu jijini Dar es Salaam jana wakiongozwa na Mwenyekiti wa chama hicho taifa, Freeman Mbowe ambaye pia ni Kiongozi wa Kambi ya Upinzani bungeni.

Katibu Mkuu wa Chadema, Dk. Willbrod Slaa, hakuweza kuhudhuria kikao hicho kwa kile kilichoelezwa kwamba alipatwa na msiba wa ndugu yake wa karibu.

Taarifa fupi ya Mbowe kwa vyombo vya habari jana jioni ilieleza kwamba viongozi hao walikutana na Rais Kikwete kuanzia saa 9:30 alasiri hadi saa 12 jioni.

"Kikao kitaendelea kesho saa 4 asubuhi (leo), taarifa kamili ni baada ya kumalizika kwa kikao," alisema Mbowe katika taarifa hiyo.

Mbowe aliongoza Kamati ndogo iliyoundwa na Kamati Kuu kwa ajili ya kwenda kuzungumza na Rais Kikwete, kuhusiana na msimamo wa chama hicho juu ya kuboresha mchakato wa kupata Katiba mpya ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania.

Viongozi wengine wa Chadema waliohudhuria kikao cha jana ni Makamu Mwenyekiti Tanzania Bara, Said Amour Arfi na Makamu Mwenyekiti Zanzibar, Said Issa Mohammed wajumbe wa Kamati Kuu ya Chadema, Profesa Mwesiga Baregu na Profesa Abdallah Safari.

Wengine ni Mbunge wa Singida Mashariki, Tundu Lissu ambaye pia ni Mnadhimu Mkuu wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni na Katibu wa Kamati hiyo.

Katika mkutano wake na waandishi wa habari mapema wiki iliyopita, Mbowe alisema mazungumzo kati ya kamati hiyo na Rais Kikwete, yanalenga kutaka kumpa msimamo, mawazo na ushauri wao namna ya kuuboresha mchakato huo.

Alisema Kamati Kuu inaamini kuwa pamoja na sheria hiyo kupitishwa, bado kuna fursa za kisiasa na kijamii katika kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya haja, nia, mchakato na misingi ya Katiba mpya.

Alisema ushiriki wa Chadema katika mchakato wa kupata katiba mpya uliowekwa na sheria hiyo, utategemea utayari wa serikali kufanya mabadiliko makubwa na ya kimsingi katika sheria hiyo kwa lengo la kujenga mwafaka wa kitaifa juu ya mchakato huo.

Katika kikao cha jana wajumbe wengine wa Chadema waliohudhuria ni Mbunge wa Ubungo, John Mnyika na Mkurugenzi wa Masuala ya Bunge na Halmashauri wa Chama hicho, John Mrema.

Kwa upande wa Serikali, mbali ya Rais Kikwete wengine waliohudhiria kikao hicho ni Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais (Mahusiano na Uratibu), Stephen Wasira, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Waziri Mkuu (Sera, Uratibu na Bunge), William Lukuvi na Waziri wa Katiba na Sheria, Celina Kombani.

Wengine ni Waziri wa Utawala Bora, Mathias Chikawe, Waziri wa Nchi, Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano), Samia Suluhu, Waziri wa Vijana, Habari, Utamaduni na Michezo, Dk. Emmanuel Nchimbi na viongozi wengine waandamizi wa serikali.

Katika kikao cha jana, baada ya viongozi wa Chadema kuwasili Ikulu, walikaribishwa na Rais Kikwete ambako pamoja na mambo mengine, walimkabidhi nyaraka zinazoeleza msimamo wa chama hicho, katika mchakato wa kuandikwa kwa Katiba Mpya.

Baada ya makabidhiano hayo, wapigapicha waliruhusiwa kupiga picha za matukio muhimu na kisha kuondoka ili kupisha mazungumzo ya kikao cha viongozi hao na Rais Kikwete.

Ikulu yasifu mazungumzo kufanyika mazingira ya kirafiki
Nayo taarifa ya Kurugenzi ya Mawasiliano Ikulu kwa vyombo vya habari imesifia mazungumzo ya pande hizo kuwa yamefanyika katika mazingira ya urafiki na ujumbe wa Chadema umewasilisha mapendekezo yake kuhusu mchakato wa kuandika Katiba Mpya ya Tanzania ambayo Serikali imeyapokea.

Ilieleza kuwa pande hizo zimekubaliana kukutana tena leo asubuhi ili kuipa nafasi Serikali kutafakari mapendekezo hayo.

Iliendelea kueleza kuwa pande hizo zimekubaliana kuwa Katiba ya sasa ni nzuri iliyolilea Taifa kwa miaka 50 iliyopita na iliyoliwezesha taifa la Tanzania kuwa na amani, utulivu na kupata maendeleo makubwa.

Vilevile zimekubaliana kuhusu umuhimu wa kutunga Katiba Mpya kama Rais Kikwete alivyoliahidi taifa wakati wa salamu zake za mwaka mpya Desemba 31, mwaka 2010 ambayo italiongoza Taifa la Tanzania kwa miaka mingine 50 ijayo.

Ilisema katika mazungumzo hayo, Kikwete aliwahakikishia wajumbe hao wa Chadema wakiongozwa na Mbowe kuwa ni dhamira yake na ya Serikali yake ni kuhakikisha kuwa Tanzania inapata Katiba mpya.

Iliongeza kuwa pande hizo zimekubaliana kuwa ni jambo muhimu sana kwa mchakato mzima wa kutungwa kwa Katiba Mpya kuendeshwa kwa namna ya kulinda na kudumisha tunu za taifa za amani, utulivu na umoja wa kitaifa.

Vilevile ilieleza kuwa pande hizo zimekubaliana kuwa mchakato huo uendeshwe kwa kuzingatia misingi ya mambo mengine muhimu kwa taifa la Tanzania kama vile kujiepusha na vitendo vya uvunjifu wa amani, kuligawa Taifa kwa misingi ya udini na ukabila ama kutugawa kwa misingi ya maeneo.

No comments:

Post a Comment