August 20, 2010

ALIKIBA AFANYA KUFURU YA MASHABIKI BILLS

MWIMBAJI wa bongo fleva, Ali Kiba, juzi alionyesha ukomavu wa kushambulia jukwaa na kupepetana vilivyo na wakali wengine, akiwamo Juma Nature. 
 Hayo yalitokea kwenye shoo maalumu iliyofanyika katika Ukumbi wa Much More, ndani ya Club Bilicanas wakati wa hafla ya kufikiwa kwa makubaliano ya kuunganisha vipindi kadhaa vya burudani vya Clouds TV na kituo cha MTVBase cha Afrika Kusini.
Kiba alipanda jukwaani baada ya Albert Mangwea ambaye naye aliwapagawisha wadau walioalikwa katika tukio hilo la kihistoria kwa Clouds. Aliimba kwa ufanisi mkubwa na baadaye, akiwa na vijana kama nane hivi, walilishambulia jukwaa na kuleta raha ya aina yake.
Mtunzi huyo wa wimbo wa Cinderella, alianza kwa kupanda jukwaani peke yake kabla ya kuomba ruksa kwa mashabiki ili vijana wake nao wapande. Aina ya uchezaji na uimbaji wa msanii huyo ulimuweka katika nafasi nzuri za wasanii wenye uwezo wa kufanya shoo nzuri, sambamba na ubunifu katika ufanyaji wake wa kazi.
Ali Kiba aliwahi kutamba na nyimbo mbalimbali, ikiwamo ile Njiwa huku pia akiwa na bahati ya kushirikishwa na wasanii wengine sambamba na kufanya shoo nyingi nje ya nchi.

No comments:

Post a Comment