November 25, 2011

Kikwete: Nimefanya kama Nyerere, Mwinyi na Mkapa

Asema hajavunja Katiba wala sheria mchakato katiba mpya    
Hakuna jinsi ya kumkwepa Rais kuwa sehemu ya mchakato    
Ahaidi anakusudia kuusaini muswada huo mapema sana

Rais Jakaya Kikwete, amesema hajavunja katiba wala sheria, bali yote aliyoyafanya katika kuandaa mchakato wa kuhuisha katiba ya nchi, ikiwamo uundwaji wa tume ya kukusanya maoni kuhusu katiba, hayatofautiani na yaliyofanywa na Marais Wastaafu; Baba wa Taifa, Hayati Mwalimu Julius Nyerere, Ali Hassan Mwinyi na Benjamin Mkapa.


Rais Kikwete alisema hayo alipozungumza na wazee wa Dar es Salaam jana, kuhusu hali ya uchumi nchini na mchakato wa kuhuisha Katiba ya nchi.


Alisema hii si mara ya kwanza kwa Tanzania kuendesha zoezi la kuhuisha Katiba ya nchi, kwani hata Mwalimu Nyerere enzi za uongozi wake, aliwahi kufanya hivyo mara tatu, ikiwamo kuunda tume kwa nyakati tofauti za kuhuisha Katiba.


Rais Kikwete alisema Mwalimu Nyerere aliihuisha Katiba ya nchi, ikiwamo kuunda tume ya kushughulikia mchakato huo mwaka 1963, 1977 na 1984.


Alisema pia mwaka 1991, Mwinyi aliunda Tume ya Jaji Francis Nyalali, iliyofanya kazi ya kukusanyan maoni juu ya mfumo wa vyama vingi vya siasa.


Alisema pia mwaka 1998, Mkapa aliunda Tume iliyoongozwa na Jaji Robert Kisanga, ambayo alisema ilileta mabadiliko makubwa ya Katiba ya nchi.


“Sasa la ajabu ni lipi kwa Rais aliyepo sasa asiunde tume ya katiba? Hoja ni nini? Amepunguza nini?” alihoji..


Katika mkutano huo uliofanyika katika ukumbi wa PTA, Viwanja vya Kimataifa vya Maonyesho ya Mwalimu Nyerere, Wilaya ya Temeke, jijini Dar es Salaam, alisema mamlaka ya Rais ya kuunda tume ya katiba ni ya Kikatiba na kuhoji: “Asipounda Rais anaiunda nani? Ataiunda vipi?” Rais Kikwete alisema rais ndiye anayepaswa kuunda tume hiyo kwa vile ndiye kiongozi wa nchi, ambaye ni kielelezo cha uwakilishi wa wananchi.


Alisema kama kutakuwa na watu, ambao watajaribu kujikusanya na kudai kuwa wao ndio wanaopasa kuandika Katiba, jambo hilo hawawezi kuachiwa, bali lazima watahojiwa walikopata mamlaka ya kufanya hivyo.


Kutokana na hilo, aliwashangaa watu wanaomfananisha na marais madikteta na kusema wanaofanya hivyo, hawawajui marais wa aina hiyo. “Mimi nimetoa uhuru wa kusema watakavyo, wanaandika watakavyo, ningekuwa rais dikteta hata hayo wasingeyasema,” alisema Rais Kikwete.


Alisema anavyofahamu yeye ni kwamba, amekuwa akisemwa sana na kwamba, lawama kubwa, ambayo amekuwa akiipata hasa katika chama chake (CCM), ni kutoa uhuru mpana kwa wanasiasa na vyombo vya habari. “Sasa nijaribu udikteta kidogo waone. Waone siku moja nasema hapa inabaki TBC (Shirika la Utangazaji Tanzania) tu, Daily News tu na gazeti la chama changu,” alisema Rais Kikwete na kusema kamwe hawezi kufanya hivyo.


Alisema watu wanaomfananisha na marais madikteta, ndio wenye moyo mdogo wa kuvumilia mawazo tofauti na wengine. “Mimi siko hivyo. Najadiliana kwa hoja. Akinishinda nasema nimeshindwa. Yote niliyoyafanya hakuna lililo nje ya Katiba na sheria…Hakuna, ambacho serikali imekosea au imevunja Katiba na sheria.”


Alisema pia kumekuwapo na upotoshaji mkubwa na uongo mwingi tangu baada ya kuhutubia na kueleza azma ya serikali ya kuanzisha mchakato huo.


Rais Kikwete alisema upotoshaji mwingine baada ya kutolewa kwa muswada wa sheria ya mabadiliko ya Katiba wa mwaka 2011 uliopitishwa na Bunge jana, ambapo baadhi ya watu walidai kuwa ndio rasimu ya Katiba yenyewe.


Aliwataka Watanzania kumpongeza, kama alifanya hivyo, Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), ambaye pia ni Mbunge wa Hai na Kiongozi wa Kambi Rasmi ya Upinzani Bungeni, Freeman Mbowe, kwa hatua yake (Rais Kikwete) ya kuanzisha mchakato huo.


Pia aliwataka Watanzania kujiandaa kutoa maoni kwenye tume hiyo mara itakapoanza kufanya kazi yake na kutaka pia watu kupewa uhuru wa kutoa maoni na wasilazimishwe kufuata mawazo ya wengine.


Kuhusu hali ya uchumi nchini, Rais Kikwete alisema athari za kiuchumi zinazoikabili dunia hivi sasa, zinaigusa pia Tanzania.


Alisema hali ya uchumi wa dunia; zikiwamo baadhi ya nchi za Ulaya Magharibi, Marekani na Japan, siyo shwari na kwamba, uchumi wao unapita katika kipindi kigumu na chenye mashaka.


Rais Kikwete alisema hali hiyo ipo pia katika nchi za Afrika Mashariki; ikiwamo Kenya na Uganda, ambako mfumuko wa bei umeongezeka, huku thamani ya fedha za nchi hizo kulinganisha na dola ya Marekani ikishuka.


Alisema kwa mfumuko wa bei Tanzania umefikia asilimia 17.9; wakati Kenya ukifikia asilimia 18.9 na Uganda ukifikia asilimia 30.5.


Pia alisema thamani ya shilingi ya Tanzania imeshuka kufikia asilimia 9.4; Kenya asilimia 6.8 na Uganda asilimia 17.4, kulinganisha dola ya Marekani.


Hata hivyo, alisema serikali imekuwa ikichukua hatua mbalimbali kukabiliana na hali hiyo, ikiwa ni pamoja na kuanzisha utaratibu wa uagizaji wa mafuta kwa pamoja unaoanza Desemba, mwaka huu.

No comments:

Post a Comment